Mabakuli Saba Ya Ghadhabu Ya Mungu

16 Kisha nikasikia sauti kuu kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage duniani yale mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”

Malaika wa kwanza akaenda akalimimina bakuli lake ardhini na madonda mabaya yenye maumivu makali yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.

Malaika wa pili akamimina bakuli lake baharini , ikawa kama damu ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.

Malaika wa tatu akamimina bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikageuka kuwa damu. Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, “Umefanya haki katika hukumu hizi uli zotoa, wewe uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu. Maana walimwaga damu ya watakatifu na manabii, na wewe umewapa damu wanywe, kama walivyostahili.” Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni za kweli na haki.!”

Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni za kweli na haki.!”

Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua nalo lika pewa nguvu za kuwachoma watu kwa moto wake mkali. Watu wakaun guzwa na moto huo nao wakalaani jina la Mungu aliyekuwa na uwezo juu ya maafa haya, wala hawakutubu na kumtukuza.

10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, na ufalme wake ukawa gizani. Watu wakauma ndimi zao kwa uchungu 11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa mau mivu yao na madonda yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.

12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa wa Efrati, maji yake yakakauka ili kuwatayarishia njia wafalme kutoka mashariki. 13 Nikaona roho wachafu waliofanana na chura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 14 Hizo ni roho za pepo zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulim wengu wote na kuwakusanya tayari kwa vita, siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. 15 “Sikiliza! Ninakuja kama mwizi! Amebarikiwa aliye macho, akiziweka tayari nguo zake ili asiende bila nguo na watu wakam wona uchi!” 16 Kisha wakawakusanya wafalme pamoja mahali ambapo huitwa “Armageddoni” kwa Kiebrania.

17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kuu ikatoka Hekaluni katika kile kiti cha enzi ikisema, “Imekwisha timia!” 18 Kukawa na miali ya umeme, sauti, ngurumo za radi na tetemeko kuu la ardhi. Hapajawahi kuwa na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu kuwapo, kwani lilikuwa tetemeko kubwa ajabu.

19 Ule mji mkuu uligawanywa katika sehemu tatu na miji yote ya mataifa ikaanguka. Mungu akakumbuka Babiloni kuu akainywesha kikombe cha divai ya hasira na ghadhabu yake. 20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana. 21 Mvua kubwa ya mawe, mawe mazito karibu kilo hamsini, ikanyesha kutoka mbinguni ikawaangu kia wanadamu. Wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya maafa ya mvua ya mawe. Kwa maana lilikuwa ni pigo kuu la kutisha.

Bakuli Zilizojazwa Ghadhabu ya Mungu

16 Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.”

Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali.

Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa.

Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu. Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu:

“Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima.
    Wewe ni Mtakatifu.
    Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya.
Watu walimwaga damu za
    watakatifu na manabii wako.
Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe.
    Hiki ndicho wanachostahili.”

Pia nikasikia madhabahu ikisema:

“Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
    hukumu zako ni za kweli na za haki.”

Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.

10 Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. 11 Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.

12 Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita. 13 Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo. 14 Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza.[a] Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu.

15 “Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.”

16 Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”.

17 Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!” 18 Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani. 19 Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu. 20 Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena. 21 Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40[b] kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana.

Footnotes

  1. 16:14 miujiza Hapa inamaanisha miujiza ya uongo. Yaani matendo ya ajabu yanayofanywa kwa nguvu za mwovu.
  2. 16:21 kilo 40 Kilo 40 (au pauni 80), ni sawa na uzito wa talanta 1.