Add parallel Print Page Options

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu

(Mt 8:28-34; Mk 5:1-20)

26 Yesu na wafuasi wake wakasafiri mpaka katika nchi walimoishi Wagerasi[a] iliyokuwa ng'ambo ya ziwa Galilaya. 27 Yesu alipotoka katika mashua, mwanaume mmoja kutoka katika mji ule alimwendea. Mtu huyu alikuwa na mapepo ndani yake. Kwa muda mrefu hakuwahi kuvaa nguo na aliishi makaburini.

28-29 Pepo aliyekuwa ndani yake alikuwa akimpagaa mara nyingi na alikuwa akifungwa gerezani, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo. Lakini kila mara aliivunja. Pepo ndani yake alikuwa anamlazimisha kwenda nje ya mji mahali pasipoishi watu. Yesu alimwamuru kumtoka mtu yule. Alipomwona Yesu, alianguka mbele yake huku akipiga kelele kwa sauti, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu Aliye Juu? Tafadhali usiniadhibu!”

30 Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?”

Mtu yule akajibu, “Jeshi.”[b] (Alisema jina lake ni “Jeshi” kwa sababu pepo wengi walikuwa wamemwingia.) 31 Pepo wale wakamsihi Yesu asiwaamuru kwenda shimoni.[c] 32 Katika kilima kile, kulikuwa kundi kubwa la nguruwe wakichungwa. Pepo wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie wale nguruwe. Hivyo Yesu akawaruhusu. 33 Pepo wakamtoka yule mtu, na kuwaingia nguruwe. Kundi lote la wale nguruwe likakimbia kutelemkia ziwani kwa kasi, nguruwe wakazama na kufia humo.

34 Wachungaji wa nguruwe walipoona lililotokea, walikimbia, wakaenda kutoa taarifa mjini na mashambani. 35 Watu wakaenda kuona lililotokea. Walipofika alipokuwa Yesu wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, akiwa na akili zake timamu; pepo walikuwa wamemtoka. Jambo hili likawaogopesha watu. 36 Wale walioona mambo haya yalivyotokea waliwaambia wengine namna Yesu alivyomponya yule mtu. 37 Watu wote waliokuwa wakiishi eneo lote la Gerasi wakamtaka Yesu aondoke kwa sababu waliogopa.

Hivyo Yesu akapanda mashua na kurudi Galilaya. 38 Mtu aliyeponywa alimsihi amfuate Yesu. Lakini Yesu akamtuma, akamwambia, 39 “Rudi nyumbani, ukawaeleze watu mambo ambayo Mungu amekutendea.”

Hivyo mtu yule alikwenda sehemu zote za mji akieleza mambo ambayo Yesu amemtendea.

Read full chapter

Footnotes

  1. 8:26 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
  2. 8:30 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
  3. 8:31 shimoni Hii ina maana kuwa ni shimo lisilo na mwisho. Ni kama shimo refu ambalo mapepo hukaa (kuzimu).