Add parallel Print Page Options

Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu

(Mk 7:1-23)

15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”

Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:

‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
    lakini mimi si wa muhimu kwao.
Ibada zao kwangu hazina maana.
    Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)

10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”

13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”

15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”

16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 15:11 unajisi Yaani, “kichafu” au “kisicho safi”, maana yake kisichokubaliwa na Mungu. Pia katika mstari wa 18,20.