Add parallel Print Page Options

Yesu Awambwa Msalabani

(Mt 27:32-44; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

21 Wakiwa njiani walikutana na mtu kutoka Kirenio aliyeitwa Simoni, akitoka vijijini kuja mjini. Yeye alikuwa baba yake Iskanda na Rufo. Wale wanajeshi wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 22 Wakamleta Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (Yaani Mahali pa Fuvu la Kichwa) 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na siki, lakini yeye alikataa kuinywa. 24 Pale wakampigilia kwa misumari msalabani. Wakagawana mavazi yake miongoni mwao nao wakayapigia kura ili kuona kila mtu atapata nini.

25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipompigilia kwa misumari msalabani. 26 Ilani ya mashtaka dhidi yake ilikuwa na maandishi haya juu yake: “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Hapo waliwapigilia msalabani wahalifu wawili pembeni mwa Yesu, mmoja kushoto kwake na mwingine kuume kwake. 28 [a]

29 Watu waliopita mahali pale walimtukana. Walitikisa vichwa vyao na kusema, “Haya! Wewe ndiye yule awezaye kuliharibu hekalu na kulijenga tena kwa siku tatu. 30 Hebu shuka msalabani na uyaokoe maisha yako.”

31 Kwa njia hiyo hiyo, viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria walimfanyia dhihaka na wakasema wao kwa wao, “Aliwaokoa wengine lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Ikiwa yeye kweli ni Masihi Mfalme wa Israeli, iinampasa ashuke sasa toka msalabani, tukiliona hilo nasi tutamwamini.” Wale wahalifu waliokuwa katika misalaba ile mingine pembeni waliosulubiwa pamoja naye nao walimtukana.

Read full chapter

Footnotes

  1. 15:28 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 28: “Na hili lilionyesha maana kamili ya Maandiko yaliyosema ‘walimweka pamoja wahalifu.’”