Add parallel Print Page Options

Yesu Awambwa Msalabani

(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

32 Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33 Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34 Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.[a] Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.

35 Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36 Askari walikaa pale ili kumlinda. 37 Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.

38 Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39 Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40 kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”

41 Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42 Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.

Read full chapter

Footnotes

  1. 27:34 nyongo Pengine ilitumika kama dawa ya kupunguza maumivu.